BOTSWANA YAMUHOJI BALOZI WA MAREKANI JUU YA KAULI YA KIBAGUZI YA TRUMP DHIDI YA BARA LA AFRIKA

Serikali ya Botswana imemshutumu Rais wa Marekani kwa kusema mataifa ya Afrika ni "machafu" na kusema tamko lake rais huyo ni la kukosa kuwajibika, la kukera na "ubaguzi wa rangi".
Bw Trump alisema hayo alipokuwa akizungumzia sera ya uhamiaji ya Marekani, ambapo alisema anafikiti watu kutoka Haiti, El Salvador na nchi za Afrika hawafai kuruhusiwa kuingia kama wahamiaji Marekani.
Botswana imesema kupitia taarifa kwamba imemwita balozi wa Marekani nchini humo kufafanua iwapo Marekani inachukulia taifa hilo la kusini mwa Afrika kama "taifa chafu" na taifa la mabwege.
Taarifa hiyo ya Botswana imesema tamko la Trump ni la kukosea heshima taifa ambalo lina urafiki wa kufana na uhusiano wa kibalozi.
Botswana imeitaka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika Sadc pamoja na Umoja wa Afrika kushutumu tamko hilo la Trump.
Bw Trump kwenye Twitter hata hivyo amejitetea na kusema hakutumia maneno hayo, lakini akasema aliyoyasema yalikuwa na "lugha kali".
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema tamko hilo la Trump ni la kushangaza, la aibu na la ubaguzi wa rangi.
Rupert Colville amesema: "Iwapo yatathibitishwa, matamshi haya ni ya kushangaza na ya aibu sana kutoka wka rais wa Marekani, nasikitika kwamba hakuna maneno mengine ya kueleza hili ila kusema kwamba ni ubaguzi wa rangi.

Source BBC

0 Comments:

Post a Comment