JAFAR AMSHUKIA JPM KWA KUTANGAZA DODOMA JIJI

WAZIRI kivuli wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa,(TAMISEMI), Jafary Michael

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU UAMUZI WA KUITANGAZA DODOMA KUWA JIJI

Itakumbukwa kuwa tarehe 26 Aprili, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli aliitangaza na kuipatia Manispaa ya Dodoma hadhi ya jiji.

Uamuzi huo umezua mjadala mkubwa miongoni mwa jamii, hasa kuhusu uhalali wa kisheria wa uamuzi huo na utaratibu uliotumika kuutangaza. Kuna hoja za msingi katika mjadala huu ambazo tunafikiri ni muhimu sana zikasikilizwa na kuzingatiwa ili kuepuka uvunjifu wa sheria na kuharibu nia njema (ya kisiasa) ambayo inaweza kuwepo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji ya Mwaka 2007 kifungu cha 7(2) na jedwali la tano la sheria hiyo, mamlaka ya kutangaza eneo la utawala na kulipandisha hadhi ya jiji yamewekwa kwa Bunge.

Aidha, uamuzi huo pia haukuzingatia utaratibu uliowekwa na Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000.

Wanaotete uamuzi wa Rais kuitangaza Dodoma kuwa jiji wanasema kuwa amefanya hivyo kwa kutumia kifungu cha 5(3) cha sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) ya mwaka 1982.

Ni vyema wakakumbuka kuwa bado sheria hiyo inamtaka Rais kuzingatia sera na taratibu zingine kabla ya kufikia uamuzi huo.

Aidha, Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 Toleo la mwaka 1997 sehemu ya 6.1.2 na 6.2.1 inaelekeza serikali kuhakikisha kuwa mipaka ya miji inawekwa kwa kuzingatia ukubwa halisi wa miji na TAMISEMI
 yanayolazimu upanuzi, ongezeko la wakazi, uwezo wa kifedha wa halmashauri husika ambayo inaomba kupanua mipaka na ushirikishwaji wa Kamati za Mipango Miji.

Pamoja na kauli hiyo ya Rais taarifa za uhakika zilizopo ni kuwa Manispaa ya Dodoma kwa maana ya Baraza la Madiwani au Kamati za Manispaa haikuhusishwa kwa namna yoyote katika mipango na hatimaye Dodoma kutangazwa kuwa jiji.

Ni lazima serikali ieleze mipaka ya Manispaa ya Dodoma kama kilomita zake za mraba au idadi ya watu inakidhi vigezo vya kuwa jiji. Na ieleze ni lini tathmini ya mipaka na kujua idadi ya watu ilifanyika ili umma wa watanzania uweze kujua.

Vilevile ni lazima tujue kama Manispaa ya Dodoma inaweza kujiendesha kwa mapato yake ya ndani kwa 95% kama ambayo sera ya Maendeleo ya Makazi na Sheria ya Mipango Miji inavyoelekeza.

Aidha, ipo miji mingine kama Manispaa ya Moshi ambayo mchakato wa maandalizi ya kuwa jiji ulishaanza kwa takriban miaka mitano iliyopita na tayari umeshatumia fedha nyingi za ndani ya halmashauri lakini kwa sababu ambazo zinaonekana za kisiasa, mchakato huo umesitishwa na Serikali hii ya awamu ya tano huku Moshi ikiwa imekidhi vigezo vyote vinavyohitajika.

Natoa mwito kwa serikali kuzingatia sheria wakati wa maamuzi yake na pia kuepuka ubaguzi wa kimaeneo wakati wa kufanya maamuzi.

Imetolewa na;

Japhary Michael (Mb)

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Ofisi ya Rais TAMISEMI
29 Aprili, 2018
DODOMA

0 Comments:

Post a Comment