UNDANI LEMA KUFUTIWA KESI YA UCHOCHEZI KISHA KUFUNGULIWA YA KUAMSHA HISIA



MAHAKAMA ya Wilaya ya Arusha imemfutia  kesi mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema,(CHADEMA) , baada ya upande wa jamhuri kushindwa kuleta shahidi wakati shauri hilo likiwa mahakamani kwa muda mrefu.

Kesi hiyo ni ya uchochezi kupitia ndoto aliyomuota Rais John Magufuli kisha kuwaeleza wananchi wa Kambi ya Fisi kata ya Ngarenaro.


Aidha muda mfupi baada ya kuachiwa mbunge huyo alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi mkoani hapa, (RCO) George Katabazi ambaye amlimtaka afike mahakama ya hakimu Mkazi Arusha ambapo alisomewa shitaka lingine la kuiamsha hisia isiyo halali kinyume cha sheria huku maelezo ya kosa yakifanana na ya kesi iliyofutwa.

Hakimu Mkazi Devota Msofe, jana  alifuta shauri hilo namba 440/2016 mbele ya wakili wa Serikali Agnes Hiyera, wakili wa utetezi, Sheki Mfinanga na mshitakiwa, Lema.

Hakimu alifikia uamuzi huo baada ya wa wakili wa Serikali, Hyera kuiomba mahakama iahirishe shauri  hilo  kwani shahidi wa saba (hakumtaja jina )aliyetakiwa kutoa ushahidi ni mgonjwa  huku akisisitiza kuwa suala la ugonjwa siyo la kupangwa bali linaweza kutokea kwa yoyote kama dharura.

Baada ya kusikiliza ombi hilo hakimu Msofe alisema," shauri ni la muda mrefu na upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi hivyo kwa sasa mahakama inamuachia mshitakiwa huru chini ya kifungu 255 kifungu kidogo cha 5 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai,".


Baada ya kuachiwa huru Lema aliondoka mahakama ya wilaya ya Arusha ambapo wakati akiwa njiani alipokea simu ya RCO Katabazi iliyomtaka afike kituo cha polisi cha Kati au mahakama ya hakimu Mkazi Arusha kwani wanaliresha upya shauri hilo mahakamani.


UPELELEZI HAUJAKAMILIKA 

Lema alisomewa shitaka la kuamsha hisia kwa njia ya isiyo halali kinyume cha sheria ambayo ilisomwa na mwanasheria wa serikali, Eiliainenyi Njiro mbele ya hakimu Mkazi, Nestory Barro.

Katika shauri hilo namba 132/2018 Lema anadaiwa kutoa maneno yaliyochochea hisia hasi kwa wananchi wa ngazi mbalimbali katika jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Maneno anayodaiwa kusema mbunge huyo yanafanana na yale ya shauri lililofutwa ambapo ilidaiwa kuwa Oktoba 22 Mwaka jana,katika maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro,katika mkutano wa hadhara anadaiwa kutoa maneno hayo.

Wakili Njiro alinukuu maneno aliyodai kuwa yalitolewa na Lema kuwa “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu,…. “Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria,mipaka ya Katiba,Rais huyo  ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu,watu watajaa vifua,wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”

Lema alidhaminiwa na Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye alikidhi vigezo vya dhamana vilivyomtaka kuwa na mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5.

Awali katika shauri lililofutwa lililotarajiwa kuendelea jana tayari mashahidi sita walishapumzika ushahidi wao  ambapo mahakama ilitupilia mbali vielelezo viwili mkanda wa video, (video cassette) na CD vilivyotaka kuwasilishwa  na shahidi wa sita upande jamhuri, Inspekta Aristides Kasigwa.

Hatua hiyo ilitokana na pingamizi lililowekwa na mawakili Lema  Januari 23, mwaka huu wakati shahidi huyo alipotaka kutoa vielelezo hivyo.

Wakili John Mallya alidai kuwa Inspekta Kasigwa ambaye anatokea idara ya uchunguzi wa picha za video na kawaida, kupiga picha za matukio ya uhalifu, kufanya uchunguzi wa ajali na sauti,  hana sifa kisheria kuwasilisha vielelezo hivyo mahakamani hapo kwani hakuhusika katika kupiga picha hizo.


Alidai shahidi ameshindwa kuonyesha mahusiano yaliyopo baina yake na vielelezo anavyotaka kuwasilisha kama sheria inavyotaka kielelezo kiwasilishwe na aliyekirekodi kwenye tukio na kukiaanda.

 Wakili mwingine wa utetezi, Sheki Mfinanga alisema shahidi huyo hastahili kuwasilisha vielelezo hivyo kwani sheria inataka shahidi anayetoa kielelezo cha vifaa vya kielektroniki anatakiwa aeleze historia ya kielelezo hicho kuanzia kilipochukuliwa mpaka kilipohamishiwa  na hatakiwi kutoa ushahidi wa kuambiwa jambo alilodai kuwa shahidi huyo hakuwa eneo iliporekodiwa mkanda huo wala hakuhusika kuusafirisha mpaka Dar es Salaam hivyo hawezi kukithi matakwa ya sheria.

Kwa upande wake wakili wa Serikali, Agnes Hyera, ambaye aliomba mahakama iharishwe kwa nusu saa ili aweze kuwasilisha hoja za majibu ambapo aliporejea alipinga hoja za mawakili wa utetezi kwa madai kuwa shahidi wao yuko sahihi kisheria kuwasilisha vielelezo hivyo kwani ndiye aliyevifanyia kazi.

"Wanasema shahidi wa nne (H 2261 Mongo) ndiyo alipaswa kuutoa mahakamani kwa kuwa ndiyo alipiga picha lakini shahidi huyo wa nne aliieleza mahakama baada ya kurekodi mkanda wa video aliupeleka kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa, (RCO), kisha ukapelekwa Dar es Salaam kwa uchunguzi," alidai wakili Hyera na kuongeza.

Shahidi wa sita (inspekta Aristides) ameeleza alipokea kielelezo hicho akakifanyia uchunguzi, akakiweka kwenye bahasha akafunga na seal  (lakiri) akairudisha kwa RCO, sasa shahidi wa nne kingemfikiaje? Shahidi wa sita ameonyesha hapa mahakamani akifungua lakiri baada ya kupatiwa kielelezo hicho kutoka ofisi ya RCO kikiwa kimefungwa,".

Hata hivyo wakili Hyera alisema wako tayari kumrejesha mahakamani hapo shahidi wa nne, PC Mongo ili awasishe kielelezo hicho cha mkanda wa video na shahidi wa sita inspekta Aristides atoe kielelezo cha CD ambacho alikiandaa.

Wakiwasilisha hoja za ziada wakili wa Lema, Mallya huku alirejea maamuzi ya mahakama ya mahakama ya Rufaa yaliyotolewa na Jaji Bernad  Luanda kwenye rufaa iliyofunguliwa na Lema dhidi ya waleta maombi, Mussa Mkakanga na wenzake wawili ambapo jaji aliamua kuwa mmiliki wa kielelezo ndiyo anapaswa kukiwasilisha mahakamani.

"Hii concept ya kielelezo kuwekwa seal na kuletwa mahakamani ni mpya kwenye masikio yangu na mahakama za jumuiya ya madola. Huyu shahidi siyo aliyepiga picha wala siyo mhifadhi nyaraka na vielelezo vya polisi. Mheshimiwa hakimu mahakama yako ni ya sheria naomba ikataze mchezo huu," alidai wakili Mallya akiomba vielelezo hivyo visipokelewe.



0 Comments:

Post a Comment