JANJA YA WAFANYABIASHARA WANAOFUNGA BIASHARA YAANIKWA

WAFANYABIASHARA wameonywa kuacha kutumia ujanja wa kutangaza kufunga biashara  kisha wanagawa bidhaa zao kwa wamachinga wawauzie ili kukwepa kulipa kodi.

Aidha wamachinga wametakiwa kuacha kufanyia biashara kwenye barabara kwani hakuna agizo lolote lililowahi kutolewa kuwaruhusu kufanya hivyo zaidi wanahatarisha maisha yao endapo gari likipata hitilafu linaweza kuwagonga.

Hayo yamesemwa jana na mkuu wa wilaya ya Arusha, Fabian Daqqaro wakati akizindua usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo mkoani hapa ambapo jumla ya wamachinga 7,300 wameshasajiliwa.

Alisema kuwa vitambulisho hivyo vitawasaidia wafanyabiashara hao kutambuliwa, hivyo vitawasaidia wasibughudhiwe wala kufuatwafuatwa huku wakichangia kukuza pato la Taifa.

"Kuna watu wanajidai wamefunga biashara wanaweka makofuli kwenye milango halafu wanawapa machinga bidhaa zao wanaozipanga mbele ya maduka yao hatutawavumilia tutashirikiana na vyombo vya dola kuwashughulikia na nyie machinga msikubali kutumika," alisisitiza DC Daqqaro.

Akiwataka Mkurugenzi wa jiji, Athumani Kihamia na Meya, Calist Lazaro kuangalia namna ya kutoa kipaumbele kwa wamachinga hao waliosajiliwa kwa kuwapatia maeneo maalum ya kufanya biashara kuzunguka stendi mpya  za mabasi zinazojengwa sanjari na maeneo maalum yaliyotengwa ndani ya jiji ambayo yatawekwa taa maalum kutumiwa na machinga hayo.

Meya wa jiji la Arusha, Lazaro aliwataka wananchi wa Arusha kubadilika na kuacha tabia ya kupenda kununua bidhaa zilizopangwa chini huku wakiacha zile za mezani jambo alilodai ndiyo linachangia ongezeko kubwa la machinga wanaopanga bidhaa chini.

"Kuna haja ya kufanya utafiti kujua ni kwa nini wateja wanapenda bidhaa zilizopangwa chini, na machinga wameshajua hilo unakuta ana bidhaa amepata mezani na nyingine chini unaona kila mara anaongeza pale chini Kwa sababu ndiyo zinanunuliwa zaidi," alisema Meya Lazaro jambo lililofanya ukumbi mzima kuangua vicheko.

Awali Kaimu Kamishina Mkuu wa mamlaka ya Mapato nchini, (TRA), Abdul Zuberi alisema kuwa zoezi hilo ni utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 inayotaka kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.

Alisema katika zoezi hilo linloendelea nchi nzima kwa kushirikiana na wengine wakiwemo Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa, (NIDA), Serikali za Mitaa, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na uhamiaji ambapo wamewatambua vikundi vya wafanyabiashara kwa kuwapatia kutambuliwa cha Taifa na namba y utambulisho wa mlipa kodi (TIN).

Zuberi alisema kitambulisho  hicho kinadumu na kutumika Kwa miaka mitatu ambapo aliwataka wafanyabiashara wadogo kujitokeza kwa wingi kuvichukua huku alitaja masharti ya kusajiliwa kuwa ni kujiunga kwenye vikundi maalum, kuwa na kitambulisho cha Taifa, kuwa na TIN na kuchangia shilingi elfu 10.

Alisema kuwa mkoani Arusha wamelenga kusajili vikundi 125 ambapo mpaka sasa wameshasajiliwa vikundi 25 vyenye wafanyabiashara 3,606 ambapo kwenye hafla hiyo walitoa vitambulisho 100.

0 Comments:

Post a Comment