Alodia Sylivesta Mitabaro (60)muuguzi wa hospitali teule ya jiji la Arusha ya St Elizabeth amefariki dunia leo asubuhi baada ya kusombwa na maji ya mvua.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Charles Mkumbo na
mganga mkuu wa Hospitali hiyo Dk Godson Kisanga kwa nyakati tofauti wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kuhuzunisha.
Dk Kisanga amesema marehemu amesombwa na maji ya mvua wakati akivuka mtaro unaopita pembezoni mwa hospitali hiyo majira ya saa moja kasoro asubuhi hatua chache kabla ya kufika hospitalini hapo.
Amesema wakati marehemu akivuka aliteleza na kusombwa na maji ya mvua na kupitishwa kwenye kalavati kadhaa; ambapo jitihada za kikosi cha zima moto na waokoaji zilikwama kumuokoa akiwa hai lakini baadaye mwili ulikutwa ukiwa umekwama kwenye tope.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo amesema limetokea leo majira ya saa moja kasoro asubuhi karibu na hospitali hiyo wakati muuguzi huyo akielekea kazini.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngarenaro Isaya Doita amesema tukio lililomkuta muguuzi huyo ni la kusikitisha huku akitoa rai kwa Wakazi wa jiji la Arusha kuchukua tahadhari hasa kwa watoto wa shule kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mwili wa marehemu umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru Mkoa wa Arusha.

0 Comments:
Post a Comment