MNYIKA ANENA BAADA YA KUTOLEWA BUNGENI

Mbunge wa Kubamba, John Mnyika 

Kwa mliotaka maelezo zaidi ya kutolewa kwangu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni "kutokuheshimu kiti", ukweli ni kuwa nimetolewa kutokana na "kiti kutokuheshimu kanuni".

Ili kupata usuli na asili ya kilichotokea leo naombeni msikilize kwanza hotuba yangu ya jana Bungeni mintaarafu kusudio langu kutaka bajeti ya Wizara ya maji isipitishwe kwanza mpaka Serikali iongeze kutoa fedha katika miradi ya maji tulizopitisha kwenye bajeti inayomalizika ya 2017/2018. Mpaka mwezi Machi serikali ilikuwa imetoa asilimia 22 tu kwenye bajeti ya maendeleo ya maji. Na asilimia 12.3 tu kwenye miradi ya umwagiliaji. Aidha, nilieleza kusudio la kutaka kuundwe kamati teule kuchunguza ufisadi kwenye miradi ya maji ambayo mingi inayotajwa kukamilika maji hayatoki na kuna matumizi mabaya.

Leo baada ya Waziri wa Fedha kutokueleza kabisa sababu ya serikali kushindwa kutoa fedha za ndani kama zilivyopitishwa na Bunge kwenye miradi ya maji wakati ikitumia fedha taslimu kununua ndege na matumizi mengine yaliyo nje ya bajeti, nilisimama ili kutoa hoja kwa majibu wa kanuni ya 69 kama nilivyoeleza kusudio jana.

Naibu Spika alinipa nafasi ya kuisoma kanuni ya 69(1) inayosema "mbunge anayependa mjadala unaoendelea juu ya hoja yoyote uahirishwe hadi wakati wa baadaye, anaweza kutoa hoja 'kwamba mjadala sasa uahirishwe' na atataja mjadala huo uahirishwe hadi wakati gani na pia atalazimika kutoa sababu kwanini anataka mjadala uahirishwe.  Badala" kiti kuheshimu kanuni " hiyo na kunipa nafasi ya kueleza sababu na kutaja tarehe, Naibu Spika akatumia vibaya kanuni 69(2) kukataa hoja hiyo nisiiwasilishe na kurusu Wizara ya maji ihitimishe mjadala ili bajeti ya Wizara ya Maji ipitishwe.  Niliposimama kutaka kanuni zifuatwe ndipo Naibu Spika alipoagiza nitoke nje.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa "kiti kutokuheshimu kanuni"  siku ya leo dhidi yangu. Awali nilitaka taarifa ya upande mmoja ya Serikali iliyotolewa na Waziri na Waziri Mkuu kuhusu uhaba wa mafuta ya kula na kupandishwa kwa bei ijadiliwe na Bunge, lakini Naibu Spika alikataa kinyume cha kanuni.

JJ Mnyika
Bungeni, Dodoma
09/05/2018

0 Comments:

Post a Comment