Hellen Kijo-Bisimba
Ufafanuzi wa Malalamiko ya Wadau dhidi ya Kituo cha Sheria na Haki za BinadamuKituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika binafsi la kujitolea na la hiari lisilo la kisiasa wala kibiashara lilosajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania mnamo mwaka 1995. Kituo kinataamali jamii yenye haki na usawa. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaendelea bila kutetereka na utekelezaji wake wa majukumu ya kulinda na kutetea haki za binadamu nchini Tanzania. Katika kujituma kwake Kituo kimeendelea kuwafikia watanzania kwa njia mbalimbali na kupitia kazi hizo Kituo kimepata mrejesho wa pongezi na hata malalamiko na tuhuma kadhaa kutoka kwa wadau.
Ili kutii mahitaji ya wadau wake na kukwepa upotoshaji ambao unaweza kusababishwa na kutokuzijibu tuhuma hizo, Kituo kimeona ni vyema kufafanua tuhuma hizo kama ifuatavyo;
1. Hoja kuwa Watetezi wa Haki za Binadamu wanatumika na nchi za magharibi
Watetezi, vikundi vya utetezi au mashirika ya utetezi wa haki za binadamu popote duniani huibuka kufuatia kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu katika jamii inayowazunguka. Nchini Tanzania hata kabla ya uhuru vimekuwepo vikundi vya watu ambavyo vilipinga ukandamizwaji wa haki uliofanywa na wakoloni. Vikundi hivi baadae vilikua na kuwa vyama vya ushirika na vingine vyama vya siasa na kuibua vuguvugu la kupigania uhuru hatimaye kupatikana kwa uhuru wa nchi.
Dhana kuwa watetezi wa haki za binadamu wanatumika na nchi za magharibi ni propaganda za upotoshaji zinazotumika na watu wasioheshimu misingi ya haki na kudidimiza juhudi za wengi kudai haki zao.
Hata hivyo misingi ya haki za binadamu ni ya Kimataifa na imetambuliwa na kulindwa na tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 pamoja na mikataba ya haki za binadamu ya mwaka 1966 inayohusu haki za kisiasa, kiraia, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ambayo yote Tanzania imeridhia, hivyo nchi inaweza kuchukuliwa hatua na Umoja wa Mataifa endapo itathibitika kukiuka haki za binadamu kwa makusudi.
2. Hoja kwamba watetezi wa haki za binadamu si wazalendo
Dhana ya uzalendo imekuwa ikitumika sana kudidimiza juhudi za kudai haki za binadamu. UZALENDO ni hali ya mtu kuipenda na kuithamini nchi yake na kuweka maslahi ya taifa lake mbele. Uzalendo unajumuisha kitendo cha mwananchi kuwa mkweli kwa taifa lake na si kuficha maovu hasa yanayoathiri watu wa taifa lake. Watetezi wa haki za binadamu ni wazalendo wa kwanza kwa taifa lao kwani hujipa jukumu la uangalizi na ulinzi wa haki za binadamu kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anafurahia nchi yake.
Dhana ya watetezi kutokuwa wazalendo ni shambulio ambalo hufanywa na watu wanaonufaika na ukandamizwaji wa haki dhidi ya watetezi wa haki.
3. Hoja kwamba watetezi wa haki za binadamu hawasifii Serikali (wamekuwa wakosoaji pekee)
Hoja hii mara nyingi huibuliwa na watu wasiopenda kukosolewa hasa waliopo katika Serikali au wanufaika wa moja kwa moja wa serikali wasiojua wajibu wa Serikali kwa wananchi. Ulinzi wa watu na stahiki zao ni jukumu la moja kwa moja la Serikali. Serikali inapaswa kutimiza wajibu wake bila kutarajia sifa au pongezi kutoka kwa wananchi. Pale Serikali inapofanya maamuzi ya busara na yenye tija inaweza kupongezwa ingawa si lazima kwani inatimiza jukumu lake kwa wananchi.
Hivyo propaganda hii kuwa watetezi wa haki za binadamu hawasifii Serikali haitoshi kuwakatisha tamaa wanaharakati wa haki za binadamu.
4. Hoja kwamba watetezi wa haki za binadamu wanaunga mkono vyama pinzani
Mara nyingi katika nchi zinazoendeshwa kwa mfumo wa demokrasia; kazi za asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu zimekuwa zikilinganishwa sana na kazi za vyama pinzani. Mbinu hii hutumiwa sana na Serikali au chama tawala katika kujaribu kukwepa hoja za msingi zinazoibuliwa na watetezi wa haki za binadamu.
Hoja hii inapingana na ukweli kwamba vyama vingi vya siasa pia hufanya utetezi wa haki za wafuasi wa vyama husika, ukiachilia mbali kuwa mara nyingine ajenda za watetezi wa haki za binadamu zinaweza pia kutumiwa na vyama vya siasa kwa lengo la kujipatia wafuasi.
5. Hoja kwamba watetezi wa haki za binadamu ni tishio kwa Amani na Usalama wa nchi
Hoja hii hutumika kuwachanganya wananchi hasa wenye uelewa mdogo juu ya haki zao, kimsingi hoja hii haizingatii ukweli kwamba asasi za kiraia hufanya tafiti za hali ya haki za binadamu na kutoa mapendekezo kwa vyombo vya dola na Serikali kwa ujumla. Hoja hii pia haizingatii ukweli kwamba asasi za kiraia ni kiunganishi muhimu cha wananchi na Serikali yao na vilevile ni jukwaa la kutatua migogoro ya wananchi kwa njia ya Amani.
Hivyo basi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kitaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza utendaji wa asasi za kiraia katika kutetea na kulinda haki za binadamu na utawala wa sheria hapa nchini. Sambamba na hilo kituo kitaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo serikali, vyama vya siasa, taasisi za dini,asasi za kijamii, wadau wa maendeleo na Wananchi wote kwa ujumla ili kufikia jamii yenye haki na usawa.
Ieleweke pia pale mtu au taasisi inapoamua kwa makusudi kupotosha ukweli kwa kiasi cha kuathiri kihasi taswira ya watetezi wa binadamu kama shirika au kwa ubinafsi wao hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa bila kusita kwani si sahihi kabisa kufanya hivyo.
Kwa kuzingatia ufafanuzi huu tunawasihi wananchi waendelee kupaza sauti bila hofu pale haki zao zinapotishiwa na kuvunjwa. Serikali haipaswi kujivua jukumu la kulinda haki za watu wake. Namna bora ya Serikali kukwepa kelele za watetezi wa haki za binadamu ni kuheshimu haki za binadamu na kuwajibika pale uvunjaji wa haki unapotokea.
Imetolewa Mei 18, 2018 na,
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji
Kwa Jamii yenye Haki na Usawa

0 Comments:
Post a Comment