WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa jana (Jumatano, Desemba 2, 2020) amefungua Kongamano la 11 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi lililoandaliwa na Bodi ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB) linalofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Katika hotuba yake Waziri Mkuu ametoa onyo kali kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi ambao bado wanaendekeza vitendo viovu kama rushwa na upendeleo na amewataka waache mara moja kwani Serikali haitomhurumia yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Pia, Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote zitekeleze maagizo ya Serikali ya kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao kwa kupitia mfumo wa kisasa wa manunuzi unaofahamika kwa jina la TANePS, ambao unasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji, uwazi, kupunguza gharama na mianya ya rushwa.
Kongamano hilo la siku tatu linatarajiwa kufungwa Desemba 4, 2020.

0 Comments:
Post a Comment