Washiriki wa mafunzo ya kuandika habari za majanga na maafa wakiwa kwenye picha ya pamoja
WAANDISHI wa habari wametakiwa kuandika habari zinazohusu majanga na maafa kwa weledi na kuepuka kuwaogopesha wananchi.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki jijini Arusha, Kaimu Mkuu wa Idara ya Habari, Rodney Mbuya kwenye hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa habari, Judith Mhina wakati akifungua mafunzo waandishi ya juu ya namna ya kukusanya na kuripoti habari za majanga na maafa.
Alisema kuwa kwa bahati mbaya au kutokuelewa waandishi wa habari wamekuwa wakikiuka misingi ya uhabarishaji hivyo kujikuta wanaripoti habari zinazowatia hofu wananchi jambo ambalo si zuri.
Mbuya aliwahimiza wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawasilisha majina ya waandishi wao wenye uweledi kwenye ofisi za idara ya habari Maelezo zilizopo Dodoma na Dar es Salaam ili waweze kupatiwa vitambulisho vitakavyosaidia kuwatambulisha pindi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
"Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uelewa juu ya namna ya kujiweka salama pindi mnapofika kwenye maeneo yaliyokumbwa na maafa na majanga msiweze kudhurika na mjue mtachukua taarifa sahihi kutoka kwa nani pia kuweza kujua ni taarifa zipi zitakazowasaidia wananchi kuchukua tahadhari zaidi na si kuwatisha," alisema Mbuya.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu idara ya menejimenti ya maafa, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na watoto, Jeshi la Polosi, Jeshi la zimamoto na uokoaji na sekta binafsi na kufadhiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, (UNESCO).
Afisa habari na Mawasiliano kutoka ofisi ya mwakilishi mkazi wa UNESCO nchini, Nancy Angulo alisema kuwa wamefadhili semina hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo 17 ya taasisi hiyo ambapo lengo la 16 linahusika na sekta ya habari.
Alisema lengo hilo linahusika na kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari na haki ya kupata taarifa pamoja ma kusimamia na kuweka kanuni na viwango katika sekta husika.
Naye , Mratibu wa maafa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Ewald Bonifasi alisema kuwa wameamua kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili waweze kuelewa namna ya kujikinga na kukabiliana na majanga kisha waielimishe jamii.
"Wandishi wa habari wakijua namna bora ya kukusanya taarifa kwenye maeneo ya majanga na kuzitangaza kwa weledi itasaidia siyo tu jamii bali hata wale wanaohusika na kushughulika na jamii kuweza kuelewa ni hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kulingana na tukio ili lisilete maafa zaidi kwa wananchi," alisema Bonifasi.
Alisema kuwa mafunzo hayo wanatarajia kuyatoa nchi nzima kwa waandishi wa habari pamoja na kamati za kushughulikia majanga na maafa za mikoa.
MWISHO



0 Comments:
Post a Comment