ASILIMIA 33 ya vifo hapa nchini husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza huku zaidi ya watu milioni 4.7 wakigundulika kuwa na magonjwa yasiyoambukiza kwa mwaka uliopita wa 2020.
Aidha, wananchi wametakiwa kubadilia mfumo wa maisha kwa kuangalia namna na aina ya vyakula wanavyokula, kwa kuepuke vyakula vyenye mafuta, chumvi au sukari nyingi bila kusahau kufanya mazoezi ya viungo.
| Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela kulia kwake Katibu Tawala mkoani hapa, |
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasioambikiza ambayo kitaifa yanafanyika Arusha kuanzia Novemba 6 mpaka 13, mwaka huu.
Alisema magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya asilimia 71 ya vifo vyote duniani ambapo mpaka mwaka 2020 watu zaidi ya milioni 57 walikufa duniani kote kutokana na magonjwa haya.
"Kwenye awamu ya sita Rais Samia Suluhu Hassan amejenga ICU, (vyumba vya kuweka wagonjwa wanaokuwa chini ya uangalizi maalum),72, X RAY 85 na CT SCAN 29 yote hiyo ni katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma sahihinua vipimo," amesema Mongela.
KWA mujibu wa wataalamu magonjwa yasiyoambukiza ni aina ya magonjwa yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Miongoni mwa magonjwa hayo ni saratani, kisukari, magonjwa ya moyo, mishipa ya damu, selimundu, magonjwa ya akili, magonjwa sugu ya njia ya hewa, magonjwa ya figo, dawa za kulevya, ajali na magonjwa ya meno na macho.
Akizungumzia maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanafanyika kitaifa mkoani hapa, RC Mongela alisema yatazinduliwa rasmi Novemba 6, mwaka huu na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa.
Alisema madhimisho hayo yatafanyika kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid ambapo kwa wiki nzima kutakuwa na maonyesho pamoja shughuli za upimaji wa afya hivyo akawataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma za vipimo pamoja na ushauri juu ya afya zao.
Alisema mawaziri wengine watakaotembelea maonyesho hayo ni pamoja na Joyce Ndalichako na Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu ambapo Waziri wa Afya, Dk Doroth Gwajima anatarajiwa kuwa mgeni rasmi siku ya kilele cha maadhimisho hayo Novemba 13, mwaka huu.
Kauli mbiuya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni badili mtindo wa maisha boresha afya.
0 Comments:
Post a Comment