SABAYA NA WENZAKE HAWAJATOKEA MAHAKAMANI



KESI ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imeshindwa kuendelea baada ya washitakiwa wote kutofika mahakamani.


Hali hiyo ilisababisha , Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda wa mahakama  ya hakimu Mkazi Arusha anayesikiliza shauri hilo namba 27/2021 kuliahirisha mpaka leo litakapoendelea kwa upande wa jamhuri kuendelea kuleta mashahidi wao.


Mara baada ya mahakama kuanza wakili wa utetezi, Moses Mahuna aliieleza mahakama kuwa  washtakiwa wote hawapo.

Kwa upande wake Wakili wa serikali mwandamizi, Ofmed Mtenga aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo kwa kuwa washitakiwa wote hawapo.


"Mheshimiwa kwa sababu washitakiwa wote hawapo na kesi ilipangwa kuendelea mfululizo, tunaomba iahirishwe hadi kesho tuendelee," aliomba Wakili Mtenga.


Wakili wa utetezi, Mahuna aliieleza mahakama hiyo kuwa hana pingamizi na ombi hilo hivyo Hakimu Mkazi, Kisinda akaahirisha shauri hilo mpaka leo saa 3:30 asubuhi.

Katika shauri hilo upande wa jamhuri umeshaleta mahakamani hapo mashahidi nane kati ya mashahidi 20 wanaotarajia kuwaleta.


Washitakiwa wengine kwenye shauri hilo ni pamoja na Enock Mnkeni, (41) maarufu  Dikdik, Watson Mwahomange, (27) maarufu Mamimungu, John Aweyo, maarufu  Mike One, Silvester  Nyengu, (26) maarufu Kicheche, Jackson Macha, (29) na Nathan Msuya, (31).


 Awali Septemba 9, mwaka huu  Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila Gervas aliwasomea mashitaka yao ambapo aliieleza mahakama kuwa washitakiwz wanakabiliwa na mashitaka matano.


Shitaka la kwanza linawakabilia washitakiwa wote saba ambalo  ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.


Akisoma maelezo ya kosa, Wakili huyo ameeleza kuwa, mnamo Januari 22, mwaka huu,  Sabaya akiwa  katika maeneo tofauti ndani ya jiji la wilaya ya Arusha  akiwa mtumishi  wa umma kwa nafasi ya mkuu wa wilaya ya Hai iliyopo mkoani Kilimanjar na anadaiwa kukiuka masharti yake ya ajira.


Sabaya anadaiwa kushirikiana na washitakiwa wenzake sita ambao si maafisa wa serikali lakini kwa makusudi kabisa walifanya vitendo vya uhalifu kwa kutumia nafasi ya Lengai ole Sabaya ambaye ni mtumishi wa umma na kujipatia fedha za Kitanzania shilingi milioni 90 kwa manufaa yao.


 Katika Shitaka la pili linalomkabili Sabaya peke yake ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na sheria ya kupambana na kuzia rushwa.


Imedaiwa mahakamani hapo kuwa  mnamo Januari 22, 2021, Sabaya akiwa kwenye maeneo ya Kwamrombo yaliyo katika kwenye jiji na wilaya ya Arusha alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kumtaka Frances Mroso ampatie shilingi milioni 90 za Kitanzania.


 


Sabaya anadaiwa kushirikiana na washitakiwa wenzake sita kama kushinikiza kupatiwa kiasi hicho cha fedha ili wasitoe taarifa za jinai dhidi ya Mrosso ambapo kwa wakati huo walikuwa wakimtuhumu kwamba alikuwa na makosa ya ukwepaji kodi.


Kosa la tatu ni kujihusisha na vitendo vya rushwa, shitaka linalomkabili Sabaya peke yake anayedaiwa kuwa mnamo Januari 22, 2021 alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa  alijipatia shilingia milioni 90 kutoka Frances Mrosso akishirikiana na washitakiwa wenzake sita katika kumshinikiza ili wasitoe taarifa ya kosa la jinai ambalo walimtuhumu nalo Mrosso.

Kosa la nne ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ambalo linamkabili Sabaya peke yake ambapo anadaiwa mnamo Januari 22, 2021 akiwa kwenye maeneo ya Kwamromboo jijini na wilayani Arusha alitumia vibaya mamlaka yake ya ukuu wa wilaya ya Hai iliyopo mkoani Kilimanjaro.


 Sabaya anadaiwa kwa makusudi kabisa alimtisha Mrosso kumfungulia mashitaka ya kukwepa kodi kinyume cha sheria za tawala za mikoa kwa madhumuni ya kujipatia  shilingi milioni 90 kwa faida yake na washitakiwa wengine sita.


 


Kosa la tano ni utakatishaji fedha  kinyume na sheria ambalo linawakabili washitakiwa wote saba ambapo wanadaiwa kuwa mnamo Januari 22, 2021 maeneo ya Kwamrombo, wote kwa pamoja walijipatia fedha kiasi cha shilingi milini 90 wakati wakijua walipokuwa wakipokea fedha hizo ni zao la vitendo vya rushwa.


Washitakiwa wote walikana mashitaka yao wote wako mahabusu kwenye gereza la Kisongo kwani mashitaka yanayowakabili hayana dhamana huku Sabaya na Nyegu wakiendelea kutumikia kifungo chao cha miaka 30 baada ya kukutwa na hatia kwenye kesi nyingine iliyokuwa ikiwakabili.




0 Comments:

Post a Comment