WADAU wa usafirishaji wameiomba Wakala wa Barabara Tanzania, (Tanroads) kuangalia ubora wa mizani zao kwani baadhi zimekuwa zinatoa vipimo vinavyotofautina.
Waliyasema hayo jana jijini hapa, kwa nyakati tofauti walipokuwa kwenye mafunzo ya siku moja ya utoaji elimu juu ya sheria ya Udhibiti Uzito wa magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya mwaka 2016 na kanuni zake yaliyoandaliwa na TANROADS.
Mwenyekiti wa Wasafirishaji wa Malori,Zainab Mnjenja alitolea mfano wa ya mizani iliyopo Iringa eneo la Wenda akidai kuwa inaongoza kwa kulalamikiwa na madereva na wamiliki wa malori.
Aliomba suala la faini ya GVN ambayo inatokana na mizigo kuzidi ikiwemo baadhi ya mizani uzito kutofautiana na kuleta sintofahamu kwa maderava na wamiliki wa malori hayo ya usafirishaji kwani gari inapopita mizani moja inaonekana na uzito sawa ila ikifika mizani inayofuata wanaambiwa wamezidisha uzito.
Mmoja wa wamiliki wa Vyombo vya usafirishaji jijini Arusha, Benedict Mberesero ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya magari ya Kimotco,alipendekeza Serikali iondoe utaratibu wa kupima mabasi ya abiria kwenye mizani kama ambavyo nchi za Kenya na Uganda zinafanya.
Mberesero alisema kuwa sheria hiyo ya Afrika mashariki inatumika kwa Nchi ya Tanzania pekee na hivyo inawaumiza wao kama wadau wa usafiri Kwa sababu abilia wao wanapowasafirisha hawapimwi uzito ila mabasi yao hulazimika kupima uzito kwenye mizani na kutozwa faini Kwa fedha za kigeni
Pia alilalamikia hatua ya kulipishwa faini Kwa Dola za kimarekani pale basi linapokuwa limezidisha uzito katika mizani jambo ambalo linawaumiza.
Awali akifungua mafunzo hayo Mhandisi wa Barabara Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Lyimo, aliwataka wadau wa safirishaji kuzingatia kanuni,sheria na taratibu za miundombinu ya barabara kama sheria ya udhiniti uzito ya EAC inavyoelekeza.
Alisema kuwa sheria hiyo ni muhimu kuzingatiwa kwani serikali inatumia gharama kubwa kujenga na kutengeneza miundombinu ya barabara ikiwemo madaraja.
Lyimo alisema kuwa endapo wamiliki wa malori,madereva na wadau kutoka Tanroads wataielewa vema sheria hiyo malalamiko mengi yatapungua ikiwemo uzito kuwa tofauti katika mizani mbalimbali
"Lazima sheria hii muielewe kwani kwa Tanzania imeanza kutumika mwezi Machi mwaka huu hivyo ni lazima mjue sheria na kanuni zake kwani kunatozo zinazokusanywa kutokana na uharibifu wa miundombinu ya barabara," alisisitiza Lyimo.
Naye Kaimu Meneja wa Shughuli za Mizani kutoka Tanroads, Mhandisi,Japhet Kivuyo alisisitiza kuwa uzito wa mizigo unaweza kuongezeka sababu ya mizigo kucheza barabarani au magari hayo kuongezwa mizigo kusisitiza hivi sasa Tanroads imepunguza malalamiko ya madereva kwa kuweka mizani maeneo mbalimbali kwa lengo la kupunguza misongamano ya magari katika mizani
Alisisitiza maderava kuacha tabia ya kuongeza mizigo kwenye malori au mabasi kwa kuwasimamisha abiria au kuwafaulisha kwalengo la kukwepa kodi
Wakati huo huo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe alisisitiza kuwa serikali imeongeza mzani wa upimaji magari eneo la Namanga Wilayani Longido na Desemba mwaka huu mzani huo utakuwa umekamilika na kuanza kutoa huduma kwa lengo la kuondoa misongamano wa magari mpaka wa Tanzania na Kenya
0 Comments:
Post a Comment