Mgogoro wa Loliondo: Mahakama Kutolea Maamuzi Novemba 22


Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imepanga kutoa maamuzi mnamo Novemba 22, 2023, kufuatia madai ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa tamko lililodaiwa kupotosha maamuzi ya Mahakama kuhusu pori la akiba Pololeti.



Waleta maombi nane wa Ngorongoro wamewasilisha maombi hayo mahakamani hapo kupitia Mawakili wao, Joseph Ole Shangay, Yonas Masiaya na Denis Moses.


Wanadai kuwa tamko hilo limekiuka maadili na linaenda kinyume na maamuzi ya Mahakama ambayo ilitoa amri ya kusimama shughuli zote ndani ya pori la akiba la Pololeti hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kumalizika mahakamani.



Wakili Masiaya ameendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa kama Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali haikubaliani na maamuzi hayo ilipaswa kukata rufaa mahakamani.


"Mahakama ina wajibu wa kulinda maamuzi yake ili Umma uendelee kuwa na Imani na mahakama, hivyo tunataka amri ya Mahakama kusimamisha shughuli za pori la akiba kutekelezwa itekelezwe ," amesisitiza wakili huyo wa utetezi.


Wakili, Masiaya amesema wanataka Mahakama ihakikishe maamuzi yake yanaheshimiwa na kufutwa kama ilivyoyatoa ya kusimamisha shughuli zote ndani ya pori hilo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.


Baada ya jaji, Mwaseba kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote aliahirisha shauri hilo npaka Novemba 22, 2023 kwa ajili ya kutoa uamuzi.



Wakati huo huo, Mahakama Kuu imepanga kusikiliza kesi nyingine Novemba 24, ambapo wakazi wa Ngorongoro, Latang  Amwakindwati, Kileo Mbilika, Namuru Kitupei, Philemon Ngulumai, Nokorenta Onyia, Metiantikw Sepena na Saitoti Parmwat wanataka kuachiwa mifugo zaidi ya 1000 iliyoshikiliwa katika pori la akiba ya Pololeti. 



Wajibu maombi kwenye shauri hilo namba 106/2023 ni pamoja na Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, na maafisa wengine wa Serikali akiwemo, Pius Rwiza, David  Mkenga, Robert Laizer na Prisca Ulomi



Wakili wa wananchi hao, Alute Mughwai, ameomba dharura ya kuachiliwa kwa mifugo hiyo, akisema imeshikiliwa kinyume cha sheria na kuwa mifugo hiyo iko hatarini kufa kwa kukosa chakula na maji.


Ameiambia mahakama kuwa endapo mifugo hiyo itakufa wateja wake ndiyo watapata hasara huku wajibu maombi wakiwa hawana madhara yoyote endapo mifugo hiyo itakufa.



Wakili wa wananchi hao Alute Mughwai, mbele ya Jaji  Mwaseba alisema wateja wake  wamewasilisha maombi ya dharura kuomba kurejeshewa Mifugo hiyo ambayo imekamatwa kinyume cha sheria.

Alisema wajibu maombi hao wamekiuka amri ya Mahakama hiyo kwa kukamata mifugo hiyo wakati kukiwa na amri ya Mahakama iliyoagiza kusitisha ukamataji wa Mifugo na watu katika eneo la Pori la Akiba Pololeti mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.


Hata hivyo , Wakili wa washitakiwa hao watano, Kapimpiti Mugalula  aliomba muda wa kuweza kuandaa na kuwasilisha hoja kinzani kabla mahakama haijapanga tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo.


Wakili Mugalula ameieleza mahakama hiyo kuwa hakuna uthibitisho kuwa wateja wake ambao wameshitakiwa binafsi ndiyo wanaoishikilia mifugo hiyo na kuongeza kuwa endapo  Mifugo imeshikiliwa hifadhini basi  kuna taratibu za kuachiwa ambazo  hazipo katika Mamlaka ya wanaolalamikiwa binafsi.


Hoja hiyo ilimuinua , Wakili Mughwai ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa wanaoshitakiwa ndio wanajua wameiweka wapi mifugo hiyo baada ya kuichukua hivyo wanaiomba Mahakama kwa kuzingatia kifungu namba 68 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai kutoa maamuzi ya dharura wakati bado kesi ya msingi inaendelea.


Wakili Mkongwe Mughwai anasaidiana na Mawakili wao, Joseph Ole Shangay, Yonas Masiaya na Denis Moses kuwatetea wananchi hao ambao walijitikeza kwa wingi mahakamani hapo.


Jaji Mwaseba amesisitiza kuwa hoja kinzani zitapokelewa Novemba 24 kabla ya kutoa uamuzi mdogo wa endapo mahakama itoe amri ya kuachiwa mifugo hiyo au la huku akiweka wazi kuwa mahakama ina lengo la kutoa maamuzi yanayotekelezeka kwa haki.

0 Comments:

Post a Comment