TARURA YAWEKEZA SHILINGI BILIONI 2.76 KATIKA TEKNOLOJIA YA UCHUNGUZI WA UDONGO

 


Uwekezaji huo kulenga kuboresha usanifu, kuongeza uimara wa barabara na madaraja na kupunguza gharama za ujenzi nchini


DODOMA — Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 2.76 katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa udongo (Geotechnical Investigation), hatua inayolenga kuimarisha usanifu, ubora na uimara wa barabara na madaraja nchini.



Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Wakala kutumia sayansi, teknolojia na tafiti za kitaalamu kuboresha ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara, huku ukisaidia kupunguza gharama zisizo za lazima.


Amesema TARURA ina jukumu la kusimamia ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabara za wilaya wenye urefu wa kilomita 144,149.18, unaojumuisha barabara za lami, changarawe na udongo.


Kwa mujibu wa Mhandisi Seff, kati ya mtandao huo, takribani kilomita 3,900 ni barabara za lami, zaidi ya kilomita 47,000 ni za changarawe na zaidi ya kilomita 92,000 ni za udongo. Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia zitakazosaidia kuboresha usanifu, ujenzi na matengenezo ya barabara hizo.


“TARURA ina jukumu la kuhakikisha kazi zinazotekelezwa zinafikia viwango vinavyotakiwa. Jukumu hili linatekelezwa kupitia Kitengo cha Tafiti na Udhibiti wa Ubora, ambacho hufanya uchunguzi wa udongo, kupima ubora wa kazi na kufanya tafiti za malighafi zinazoweza kutumika katika ujenzi wa barabara,” amesema.


Ameeleza kuwa vifaa hivyo vitawezesha Wakala kupata taarifa sahihi kuhusu sifa za udongo na uwezo wake wa kubeba mizigo, taarifa ambazo ni muhimu katika usanifu wa barabara na madaraja yenye uimara na uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.


Aidha, amesema teknolojia hiyo itaimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani kufanya tafiti kwa ufanisi, kutambua malighafi zinazofaa kwa ujenzi na kubaini mbinu zinazoweza kupunguza gharama za miradi bila kuathiri ubora wa miundombinu.


TARURA YAZIIMARISHA MAABARA ZA UCHUNGUZI


Mhandisi Seff amesema TARURA ina maabara kuu jijini Dodoma na maabara nyingine zaidi ya 15 katika mikoa mbalimbali nchini, zinazohusika na kupima udongo, kuthibitisha ubora wa kazi za ujenzi na kufanya tafiti za malighafi zinazopatikana katika maeneo mbalimbali.


Amebainisha kuwa wakati mwingine malighafi zinazotumika katika ujenzi wa barabara hupatikana mbali na maeneo ya miradi, hali inayoweza kuongeza gharama za usafirishaji.


Kupitia tafiti zinazofanywa na maabara hizo, TARURA huchunguza malighafi zinazopatikana karibu na maeneo ya miradi ili kubaini kama zinafaa kutumika na zinakidhi viwango vinavyotakiwa. Hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza gharama za usafirishaji na matumizi yasiyo ya lazima katika utekelezaji wa miradi.


Amesisitiza kuwa maabara hizo zina jukumu muhimu katika kuthibitisha ubora wa udongo, malighafi na kazi za ujenzi, kwa lengo la kuimarisha uimara wa miundombinu na kuhakikisha fedha zinazotumika katika miradi ya barabara zinatoa thamani iliyokusudiwa.


Katika kuimarisha matumizi ya huduma hizo, Mtendaji Mkuu huyo amewakaribisha makandarasi na wahandisi washauri wanaotekeleza miradi ya TARURA na taasisi nyingine kutumia huduma za maabara za Wakala zilizopo Dodoma na katika mikoa mbalimbali nchini.


Amesema maabara hizo zina vifaa vya kisasa vinavyoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya ujenzi, huku wataalamu wa TARURA wakiwa wamepatiwa mafunzo yanayowawezesha kufanya uchunguzi na tafiti za udongo kwa ufanisi.


Ameongeza kuwa TARURA itaendelea kuongeza vifaa na kuimarisha maabara zilizopo mikoani ili kupanua wigo wa huduma, kurahisisha upatikanaji wa vipimo na kuimarisha udhibiti wa ubora wa miradi ya barabara na madaraja.


Uwekezaji huo unalenga kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika usimamizi wa miundombinu ya barabara, kupunguza gharama zisizo za lazima na kuongeza ubora na uimara wa barabara zinazochochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.

0 Comments:

Post a Comment