DKT. MWIGULU AZINDUA KITAMBULISHO CHA TAIFA KILICHOBORESHWA

 


WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Kitambulisho cha Taifa kilichoboreshwa (toleo la mwaka 2026), akisisitiza kuwa uwekezaji huo unapaswa kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuondoa usumbufu kwa wananchi.
W



Katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Stendi ya Zamani ya Mailimoja, Kibaha mkoani Pwani, Waziri Mkuu pia amezindua teknolojia mpya ya uzalishaji wa vitambulisho, programu tumizi ya NIDA Wallet, pamoja na magari 10 ya huduma za usajili.


Amesema maboresho hayo yanafungua milango ya kuunganisha huduma mbalimbali kupitia utambulisho mmoja, hatua itakayopunguza ulazima wa wananchi kubeba vitambulisho vingi katika shughuli zao za kila siku.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha uwekezaji huu unaleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya kila siku ya Mtanzania,” amesisitiza Dkt. Mwigulu, huku akielekeza kuwa kila Mtanzania mwenye sifa apate kitambulisho kwa wakati bila urasimu.


Aidha, amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha uwekezaji huo, akibainisha kuwa matumizi ya teknolojia yanapaswa kuboresha utoaji wa huduma, kuimarisha utawala bora na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Maboresho ya Kiufundi na Kidijitali
Akifafanua kuhusu maboresho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, amesema Serikali imewekeza zaidi ya Sh. bilioni 30 kununua kadi mpya na mashine tano za kisasa zenye uwezo wa pamoja wa kuzalisha vitambulisho 2,800 kwa saa.
Amesema mashine hizo zinatumia teknolojia ya mionzi ya leza (laser engraving) kuchora taarifa na picha ndani ya tabaka za kadi badala ya uchapishaji wa wino wa kawaida, hatua inayoongeza uimara wa kadi na kudhibiti mianya ya kughushi.
Vilevile, ameeleza kuwa nafasi za programu za kidijitali (applets) zinazoweza kuunganishwa kwenye kadi zimeongezwa kutoka nne hadi nane ili kuruhusu matumizi mapana zaidi. Uunganishaji wa huduma kama bima ya afya, leseni za udereva na usafiri utafanyika kwa awamu kulingana na utayari wa mifumo, makubaliano ya kitaasisi na matakwa ya kisheria.
“Lengo si kuongeza teknolojia kwa ajili ya teknolojia, bali ni kumwezesha mwananchi kutumia utambulisho wake katika huduma mbalimbali kwa usalama na urahisi zaidi,” amefafanua Kaji.
Kuhusu NIDA Wallet, amesema ni programu tumizi inayomwezesha mwananchi kuhifadhi utambulisho wake kidijitali kwenye simu janja na kuutumia kuthibitisha taarifa zake anapopata huduma, kadiri mifumo ya taasisi husika itakavyounganishwa.
Uhalali wa Vitambulisho vya Zamani
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa wito kwa wananchi kutokuwa na hofu, akisisitiza kuwa uzinduzi huo hauondoi uhalali wa vitambulisho vya awali.
“Hauna sababu ya kwenda kubadilisha kitambulisho chako cha zamani kwenda kupata kipya kama hakuna sababu yoyote ya msingi,” amesema Katambi, huku akiwahimiza wananchi waliojisajili kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao vilivyo tayari.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Paschal Inyasi Chinyele, amepongeza hatua hiyo, akisisitiza umuhimu wa kulinda taarifa binafsi za wananchi, kuimarisha ushirikiano baina ya NIDA na taasisi nyingine, pamoja na kuhakikisha uendelevu wa teknolojia hiyo.

0 Comments:

Post a Comment