MADIWANI WA CHADEMA WAMSHUKIA DC MONGELA WAMTAKA ASIINGILIE KAZI ZA MKURUGENZI WA JIJI

MADIWANI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) jijini hapa pamoja na mbunge, Godbless Lema, wamemtaka Mkuu wa wilaya ya Arusha, John Mongela kuacha kuingilia shughuli za utendaji ambazo kisheria ziko chini ya  mkurugenzi wa jiji,Juma Iddi.

 

Aidha wamewataka wamachinga walionyang'anywa mali zao na mgambo wakati wa operesheni safisha jiji, wafike kwenye ofisi za  jiji ambapo wataongoza zoezi la kuwarejeshea mali zao kuanzia majira ya asubuhi muda wa kazi unapoanza.

Pia wamemtuhumu Mkuu huyo wa Wilaya kuhusika na vitendo vya ubadhirifu wa fedha zinazotokana na mapato ya ushuru kwenye masoko mbalimbali ya jiji ambapo tayari suala hilo wamelifikisha kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini, (TAKUKURU).

 

Waliyasema hayo jana wakati wakiongea na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Kibo Palace ambapo walikuwa madiwani wote wa Chadema, akiwemo Naibu Meya, Prosper Msofe, Mbunge Lema na viongozi wa Chama hicho ngazi ya wilaya.

 

Lema alisema kuwa hawapingi  jiji kuwa safi kwani ni agenda ya Chadema na inatekelezwa kwenye maeneo ambayo chama hicho kinaongoza halamshauri ila wanachokataa ni zoezi hilo kutekelezwa kwa ukatili mkubwa huku likishindwa kusimamia misingi ya haki na heshima ya utu.

 

Alisema kuwa wamekaa kama madiwani wameona Mkurugenzi wa jiji anaingiliwa sana kwenye masuala ya utendaji na Mkuu wa wilaya jambo alilodai kuwa linathibitishwa na tukio la hivi karibuni ambapo madiwani na mkurugenzi walikaa na kuamua kuwasimamisha kazi mgambo ili kupisha uchunguzi wa tukio la Diwani Ephata Nanyaro na Naibu Meya, Msofe kupigwa .

 

Mbunge huyo wa Arusha Mjini alisema kuwa katika hali isiyotarajiwa Mkuu wa Wilaya alienda kwenye vyombo vya habari akawatangazia mgambo kurudi kazini jambo alilosema kuwa si sahihi kwani mgambo wanaajiriwa na mkurugenzi chini ya idara ya sheria hivyo maamuzi ya madiwani na mkurugenzi hayakuwa sahihi kupuuzwa na DC.

 

"Tatizo la wamachinga ni kubwa kuliko watu waanavyofikiria, huwezi kulimaliza kwa siku moja , linahitaji mkakati madhubuti , hapa Arusha tuna maeneo makubwa ambayo ni mali za jiji lakini yaliuzwa kifisadi kama lile lililopo pale pembeni ya soko la kilombero ,Rais anaweza kutumia mamlaka yake kwa kufuta ile hati , eneo lile likatumika kwatengenezea miundombinu itakayowezesha wamachinga wengi kuendesha shughuli zao," alisema Lema.

0 Comments:

Post a Comment