Sote tuwe na umoja..

"Sote tuwe na Umoja" (rej. Yn 17:21)
UTANGULIZI:
Ndugu wapendwa, tunapohitimisha kipindi cha Kwaresima kilichokuwa na
ujumbe: "Ukweli utawaweka huru" (Yn. 8: 32), tunawaletea ujumbe wa
"Umoja" ili kuongeza msisitizo kwenye ujumbe wetu wa Kwaresma.
Tunaitwa kukubali kuwa umoja ni ukweli msingi wa kila mafanikio ya
jumuiya ya mwanadamu.
Ufufuko ni Pasaka inayomaanisha kivuko au kupita kwa Wayahudi toka
kwenye matatizo ya utumwa hadi uhuru kamili. Kwa Wakristo ni kuvuka
kutoka utumwa wa fikra za kifo (dhambi) hadi uhuru kamili wa ufufuko
wetu na Bwana Yesu. Kwahiyo, furaha za Pasaka zinapaswa kusheheni
shukurani za dhati kwa zawadi nyingi alizotujalia Mungu Muumba wetu
tokea mwanzo na hasa nyakati hizi katika mwanga wa Ufufuko wa Kristo.
Adhimisho la Pasaka litawaliwe na furaha, amani na matumaini makuu
yaliyoletwa kwa Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Mtume Paulo
anatuambia: "Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu
Kristo" (1Kor. 15:57).
Wakati dhambi na kifo husababisha kujitenga; uhuru, furaha na amani
husababisha kuungana. Ndivyo ilivyotokea kwa Adamu na Eva. Walipokuwa
bila dhambi walikuwa huru, wenye furaha, amani na umoja na Mungu.
Walipotenda dhambi walimkimbia Mungu, wakatafuta kujificha. Hata wao
wenyewe walioneana aibu na hatimaye wakafukuzwa kutoka kwenye bustani
ya Edeni (Mwa. 2:25; 3:7-8, 23-24).
1.Ndugu zetu katika Kristo, "Amani iwe Kwenu" (Yn. 20:19). Wakati huu
wa Pasaka, wakati ambao pia mchakato wa kuandika Katiba ya nchi yetu
unaendelea, hatuwezi kuacha kutafakari kwa dhati juu ya umoja wetu
sisi Watanzania. Bila shaka, moja ya mihimili mikubwa ya umoja wa
kitaifa ni uongozi bora.
Mwenyezi Mungu aliwatoa watu wake utumwani Misri na kuwaweka huru kwa
kuwateulia viongozi miongoni mwao. Kiongozi wa kwanza alikuwa Musa
(Kut. 3:10).
• Chini ya uongozi wa Musa Wayahudi walichukua muda mrefu kujenga
umoja na uelewa, kwamba walikuwa watu wa Mungu na walipaswa kumtambua
kiongozi wao kama mteule wa Mungu (Kut. 16:3; 17:4.
• Katika kutangatanga kwao jangwani, iliwachukua pia muda mrefu
kutambua uovu wao na kujitakasa dhidi ya dhambi zao (Kut. 32:1-14).
• Hata wakiwa tayari katika nchi waliyoahidiwa hawakuacha machukizo
yao kwa Mungu pamoja na kukanywa mara kwa mara na Manabii wake
Mwenyezi Mungu (Amu. 2:11-13).
Wakati ulipowadia, Mungu alimtuma Mwanae Yesu Kristo kujenga Utawala
wa Mungu juu ya msingi wa imani na ukweli (Gal. 4:4):
• Imani kwa Mungu na imani baina ya watu wenyewe – kuaminiana – ndio
msingi wa Utawala wa Mungu (2Thes. 2:13-17).
• Lakini kutokana na udhaifu wa kibinadamu, mara nyingi tunavunja
umoja wetu na Mungu na kati yetu wenyewe kwa kiwango cha kutotaka
kuishi pamoja; tunabaguana na hatutendeani haki (Mwa. 4:7-8).
Katika ulimwengu wa leo, tunashuhudia madhara ya utengano wa namna
nyingi. Dhambi nyingi za binadamu zinasababisha mifarakano na vita.
Hayo ni matukio ya kila mara katika nchi nyingi ulimwenguni na hasa
kwetu Afrika. Hata historia yetu wenyewe ina matukio mengi ya jamii
kufarakana na kujizamisha katika vita.
• Mababu zetu walipitia maisha marefu ya kuhamahama na kuchukuliwa
utumwani na wengine kubaki watwana na watawaliwa wa kikoloni kwa
vipindi virefu kabla ya kujipatia uhuru wa kujitawala.
• Tulipopata uhuru, tulijifunza kujenga umoja katika tofauti zetu
kubwa za kikabila na kufikia taifa moja.
• Tulichukua hatua kubwa kuunganisha nchi mbili huru, Tanganyika na
Zanzibar, na kuifanya kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ikiwa kielelezo kwa Bara la Afrika cha kujenga umoja.

2.Hatua zote hizo tulizopitia na tulizochukua kwa makusudi kabisa,
tulikuwa na nia na utashi wa kuwa wamoja. Tulitaka kujenga maendeleo
ya pamoja na mafanikio ya kila Mtanzania kufikia maisha bora. Jitihada
hizi njema zimekuwepo kwa miaka hamsini iliyopita. Tumefanikisha mambo
mengi katika umoja wetu ambao unatusukuma kumshukuru Mungu. Kwa muda
mrefu umoja wa Watanzania umeonekana kwa mataifa mengine kuwa ni
kielelezo cha umoja wa kitaifa wa hali ya juu sana. Ni umoja uliokua
kufikia kiasi cha kufuta tofauti za awali za mataifa yaliyohusika
kuunda umoja.
Tunamshukru mwenyezi Mungu kwa kuifanya Nchi yetu kuwa kimbilio la
waliokata tamaa. Tanzania imewapa wakimbizi mahali salama pa kuishi
pamoja na Watanzania. Chini ya Jamhuhuri ya Muungano wa Tanzania,
waliokuwa bado chini ya wakoloni, waliandaliwa kujikomboa na kuwa
mataifa huru.
Pamoja na mafanikio hayo makubwa, zimejitokeza dosari kadhaa katika
umoja zilizofanya umoja wetu upoteze baadhi ya sifa zake za awali.
Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari
iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndio ukweli. Baadhi
ya Watanzania wanafikiri kuwa umoja unaofuta tofauti haufai ila umoja
unaosisitiza tofauti kama ulivyo umoja wa kikanda (kama ilivyo SADC,
ECOWAS, n.k) ndio unafaa! Wakati mataifa mengine yanatamani umoja
unaofanana na ule umoja wetu wa awali, baadhi yetu tunatamani kurudi
nyuma kwenye umoja wa mpito!
Kutokana na mapungufu yaliyodhihirika ndani ya mafanikio yetu, umuhimu
wa kufanya marekebisho ulidhihirika. Ni kwa sababu hiyo, watu wengi
walitaka na wanataka mabadiliko au mageuzi ya msingi sana. Kwa msukumo
huo ndio sababu tuliingia katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
3.Kazi ya kuandika Katiba si nyepesi na yataka umakini mkubwa.
Haishangazi sana tunapojionea mivutano na migongano ya hoja kutoka kwa
makundi kinzani katika nchi moja. Mawazo ya wengi yamewasilishwa
kisheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kujadaliwa na
Bunge Maalum la Katiba (BMK). Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu
yakijaribu kushinikiza kuingizwa matakwa yake kwenye Katiba kwa njia
zozote zile ili kujihakikishia kuendelea kulinda maslahi yake ya
kisiasa. Wajumbe wa Bunge Maalum Katiba wanazozana,
wanakashifiana,wanatukanana na hawataki kuachana na itikadi za kisiasa
ili kufikia muafaka katika masuala muhimu yatakayowahakikishia raia wa
kawaida kushiriki kwenye fursa za maendeleo kwa manufaa ya wote. Hayo
lakini yasitukatishe tamaa na kujiona kama tu watu wa kushindwa wakati
tukiwa bado kwenye mchakato mrefu wa kujipatia jukwaa jipya kwa
mustakabali wa taifa letu Tanzania.
Tushirikiane na wote wenye nia njema kupambana na nguvu za maovu na
ubinafsi na kuachana na itikadi za kisiasa na matakwa ya kiuchumi ya
matabaka ya walio nacho ili kupigania haki za wanyonge. Tuandae Katiba
ambayo itatupatia misingi imara ya maadili itakayotuongoza kupigana
dhidi ya ubinafsi na ufisadi, na kutetea haki za binadamu kwa wote.
Vigezo vyote muhimu kwa maisha ya mshikamano kitaifa vimeandikwa
katika Rasimu ya Katiba Sura ya 1 hadi ya 5. Tukisha kukubaliana na
yaliyomo katika sura hizo, muundo wowote wa Serikali unawezekana kwa
kuzingatia kanuni za uwiano wa madaraka na wajibu wa mihimili mitatu
ya Dola kwa mujibu wa Sura za 8 hadi 15.
Ili tufikie lengo letu la kuwa na Katiba bora katika hatua tuliyofikia
ya mchakato wa Katiba Mpya yatubidi kuzingatia yafuatayo:
• Kuheshimu kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuitumia kama
ilivyokusudiwa na sheria iliyoiweka.
• Kuwa na nia njema ya kweli ya kutafuta suluhisho la matatizo mengi
ya utendaji katika Dola zilizopo katika Muungano.
• Kuwa na hamu ya kujitoa kwa taifa na kulitumikia kwa moyo bila
kutawaliwa na ubinafsi au kujipendelea kiinchi na kiukanda kwa
madhumuni ya kuboresha maisha ya Watanzania wote.
• Chaguo la muundo wa Dola, sharti liongozwe na malengo na madhumuni
ya umoja wetu wa kutaka tuishi kwa mshikamano wa dhati. Uchaguzi wa
muuungano wa serikali moja, mbili au tatu sharti ufanywe kwa dhamiri
safi iliyo na uelewa uliochambua matatizo yaliyopo ya Muungano na
kuridhia mfumo utakaosuluhisha matatizo hayo pasipo mashaka yoyote.
4.Baada ya kutafakari historia ya ukombozi wa mwanadamu kwa ufupi na
hatua Watanzania tuliyofikia katika uhuru wetu wakati huu wa adhimisho
la Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo mwaka 2014, tungependa kwa namna
ya pekee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumvuvia Rais Jakaya M. Kikwete
ujasiri wa kuamua kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kisheria katika wakati muafaka.
Kwa mchakato huo wa Katiba, kupitia Tume yake Huru, Watanzania
wamepata fursa ya kusema kila jambo lililowaelemea maishani na
kuainisha namna wanavyotaka kujitawala. Wakati ulikuwa mwafaka kwa
sababu kulikuwa na manung'uniko mengi ya ukiukwaji wa Katiba ya sasa
ambayo hayakuweza kujibiwa na Serikali zilizopo. Hatua ya kuamua
kuyakabili hayo kwa sheria ya Kurekebisha Katiba iliwapa wananchi
fursa ya kutoa maoni yao bila mizozo na machafuko.


5.Tume ya Mabadiliko ya Katiba imewasilisha kwenye Bunge Maalum la
Katiba Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni huru ya watu binafsi na
makundi mbali mbali zikiwemo taasisi za dini, mamlaka za kiserikali na
asasi huru za kiraia. Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalum la Katiba
kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa
za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano,
mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia
wa Tanzania.
HITIMISHO
Ndugu wapendwa,
Wakati huu wa Pasaka, tuendelee kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili
wajumbe wawe wazingatifu wa matakwa na matarajio ya Watanzania
yalivyoainishwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba na Tume ya mabadiliko
ya Katiba kwa kuheshimu maoni ya Watanzania na kuboresha maoni hayo
kwa hekima na busara ili kulinda mstakabali wa Taifa letu; Tanzania
yenye amani kwa ustawi wa watu wote.
"Ingekuwa heri leo msikie sauti hii; msifanye migumu mioyo yenu".
(rej. Zab 95:7-8)
Tuombe:
Ee Bwana, katika upendo wako uwape neema watu wa taifa lako, waishio
Tanzania. Katika upendo wako ujenge tena nguzo za imani, matumaini na
mapendo katika mji nchi yetu. Watanzania wakiwa na imani, matumaini na
mapendo ya haki utapendezwa na sadaka wakutoleazo; kila mtu akijitolea
yeye mwenyewe kwako kama sadaka safi juu ya altare, pamoja na katika
Kristo Mfufuka aliye katika Ekaristi.
Mama Bikira Maria atuombee ili ndani yetu uzaliwe upya uaminifu
unaotupa uwezo wa kutangaza kazi kuu ya Mungu. Tunaomba hayo kwa njia
ya Kristo Bwana wetu. Amina.
Amani ya Kristo Mfufuka iwe nanyi

Ni sisi Maaskofu wenu:
1. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania, Askofu wa Iringa
2. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam
3. Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha
4. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora/Kigoma Msimamizi
5. Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro
6. Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara
7. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi, Ofm Cap, Mwanza,/Shinyanga
8. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi
9. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga
10. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge
11. Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya
12. Mhashamu Askofu Augustino Shao, Cssp, Zanzibar
13. Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga
14. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara
15. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba /Singida Msimamizi
16. Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba
17. Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita/Askofu Mkuu Mteule Songea
18. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, OSS, Kahama
19. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe
20. Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi
21. Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu
22. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma
23. Mhashamu Askofu Issac Amani, Moshi
24. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga
25. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, Same
26. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara
27. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam
28. Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda
29. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Mpanda /Dodoma
30. Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa
31. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga
32. Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Dar es Salaam

--
____________________
In real life it doesn't matter who we are better than, it only matters
that we are better than we were.
Mob: +255 719481111/+255754078089

0 Comments:

Post a Comment