| Kaka yake Tundu Lissu, Alute Mughwai |
FAMILIA ya Rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika na mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA),Tundu Lissu, imeweka imemtaka waziri wa afya aeleze maombi wanayotakiwa kuwasilisha serikalini ni ya mkopo, punguzo la mkopo au msaada wa matibabu.
Kaka wa mwanasiasa huyo machachari, Alute Mughwai ambaye naye ni mwanasheria ameyasema hayo leo kwenye mkutano wa nusu mwaka wa TLS uliofanyika jijini Arusha.
Amesema kwa sasa wataendelea kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), TLS na wasamaria wema wanaochangishana kwa njia mbalimbali kufanikisha kupata fedha za kugharamia matibabu ya ndugu yao.
Msemaji huyo wa familia hiyo alisema hawajaelewa tamko la Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto , Ummy Mwalimu anawataka waombe nini wakati Lissu kwa nafasi yake ya ubunge anastahili na haki zote za kutibiwa na serikali hasa ikizingatiwa alishambuliwa na kuumizwa akiwa katika eneo lake la kazi.
"Familia haielewi masharti haya yana lengo gani, kwanza hatujui mgonjwa aombe mkopo, nafuu ya mkopo au ya msaada wa matibabu. Hatuelewi na kwa sasa hatutaki masharti katika kumrejesha ndugu yetu katika afya yake," alisema kaka mkubwa huyo wa Lissu na kuongeza.
“Tunashirikiana tangu mwanzo wa tukio hili na Chadema, TLS na wasamaria ambao wengi ni wananchi na watu wengine wa kawaida wacha tusiwakatishe tamaa hawa waliojitokeza mwanzo kuwa nasi hawa wenye masharti wasubiri,".
Hivi karibuni Waziri Mwalimu alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa serikali iko tayari kugharamia matibabu ya Rais huyo wa TLS nchi yoyote duniani endapo atapokea maombi rasmi kutoka kwa familia.
0 Comments:
Post a Comment