MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, leo imeshindwa kutoa uamuzi kwenye rufaa ya mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), baada ya Jaji, Dkt Modester Opiyo, anayesikikiza rufaa hiyo kuwa kwenye vikao vya usikilizaji wa kesi za mauaji na madawa ya kulevya vinavyoendelea mahakamani hapo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angelo Rumisha aliahirisha shauri hilo mpaka Novemba 27, mwaka huu saa tatu asubuhi utapotolewa uamuzi huo.
kwenye shauri hilo Lema anapinga uamuzi uliotolewa na mahakama ya hakimu mkazi uliyekataa shauri lake analodaiwa kuhamasisha maandamano ya ukuta lisiende kusikilizwa mahakama Kuu.
Shauri hilo la rufaa ya hiyo ya jinai namba 48/2017 limesikikizwa kwa njia ya maandishi ambapo Lema anawakilishwa na mawakili Sheki Mfinanga huku upande wa Jamhuri ukiwa namawakili wa Serikali, Innocent Njau na Khaliki Nuda.
Katika shauri hilo mawakili wa Lema waliwasilisha mahakamani hapo hoja zake za rufaa kwa njia ya maandishi Agosti 30, mwaka huu ambapo upande wa Jamhuri waliwasilisha hoja za majibu Septemba 13, huu.
KILICHOPELEKEA LEMA KUKATA RUFAA
Uamuzi mdogo uliokatiwa rufaa ulitolewa februari 8, mwaka huu na Hakimu Mkazi,Bernad Nganga, wa mahakama ya hakimu Mkazi Arusha, kwenye shauri la jinai namba 352/2016 ambaye alitupa pingamizi lililowasilishwa na mawakili wa Lema wakitaka shauri hilo likasikilizwe na majaji watatu kutokana na hati ya mashitaka kujumuisha masuala ya kikatiba.
Akisoma uamuzi huo mdogo, Hakimu Mkazi, Nganga alisema kuwa mara baada ya kupitia hoja za pande zote mbili ameamua shauri hilo liendelee kwenye mahakama hiyo huku akidai kuwa endapo kuna masuala ya kikatiba yatakosa majibu basi itawanufaisha upande wa utetezi.
"Ushahidi wa Jamhuri kushindwa kutolewa hautakuwa na madhara kwa mshitakiwa bali utamfaidisha na hoja ya shauri kuwa na masuala ya kikatiba, hoja hiyo huwezi kuitambua kwa kuangalia vifungu alivyoshitakiwa navyo mshitakiwa na kama ni hivyo hoja hiyo iletwe wakati wa utetezi kama kesi itafika hatua ya utetezi.
"Pingamizi zinatupiliwa mbali na mahakama hii haijaona haina uwezo wa kusikiliza hivyo tutaendelea na kesi ya msingi," alisema hakimu Nganga akihitimisha uamuzi wake.
Alisema, alipitia hati ya mashitaka inayoeleza kuwa Lema anashitakiwa kwa kosa la kushawishi kutenda kosa kinyume na kifungu cha 390 na cha 35 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambapo anadaiwa kuhamasisha watu kufanya kusanyiko na maandamano isivyo halali.
"Baada ya kupitia hati hiyo na kwa mujibu wa kifungu cha 390 kinaelezea mtu akihusika na kushawishi kosa,hata kama halina madhara huyo mtu ni mkosaji.Kifungu cha 35 kinaelezea iwapo mtu akikutwa na hatiani kwa kosa hilo adhabu yake ni kifungo cha miaka miwili au faini au vyote viwili kwa pamoja," alisisitiza hakimu huyo
Baada ya uamuzi huo wakili wa Lema, Sheki Mfinanga aliwasilisha kusudio la kukata rufaa kwa njia ya mdomo kwa kile alichoeleza kuwa hawajaridhika na uamuzi huo na kuomba kuwasilisha notisi hiyo ambayo ina nguvu sawa na rufaa huku akiomba kupatiwa mwenendo wa kesi hiyo pamoja na uamuzi huo mdogo ili waweze kuandaa rufaa hiyo na kuwasilisha Mahakama Kuu.
"Tunaupinga uamuzi huu ulioutoa na tunaomba kuwasilisha notisi ya kukata rufaa ambayo ina nguvu sawa na rufaa na tunaomba shauri lisiendelee kwanza mpaka Mahakama Kuu ikasikilize rufaa yetu dhidi ya uamuzi huu," alisema Mfinanga.
0 Comments:
Post a Comment