CHADEMA WAADHIMISHA MIAKA SABA TANGU MAUAJI YA ARUSHA, KATIBA MPYA NA TUME HURU YA UCHAGUZI VYAWA KIPAUMBELE

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
CHADEMA KANDA YA KASKAZINI
(TANGA, KILIMANJARO, ARUSHA & MANYARA)

TAARIFA KWA UMMA
5 JANUARI 2015

TANZANIA INAHITAJI KATIBA MPYA YA WANANCHI NA TUME HURU YA UCHAGUZI
MIAKA SABA TOKA MAUAJI YA TAREHE 5 JANUARI 2011 ARUSHA

Huu ni mwaka wa SABA tangu kutokea kwa mauaji ambayo leo yanatupa kumbukumbu chungu ya tukio lilitokea katika Jiji la Arusha na kupekea kuuwawa kwa wananchi watatu walioripotiwa Denis Shirima, George Njuguna (Mfanyabiashara Mkenya ambaye alikuwa ameshuka kutoka Namanga kwa safari ya kibiashara) na Omari Hamisi. Pamoja na wengi sana kujeruhiwa kwa risasi za moto, mabomu yaliyofyatuliwa na polisi na kugongwa na magari. Arusha Mjini ilishuhudia damu ikimwagika, hospitali za jijini Arusha zilipokea mamia ya wanaume, vijana, wanawake hadi watoto waliopigwa kwa risasi pasipo na hatia hata kidogo.

Mauaji haya yalitokea wakati wananchi wa Arusha walipokuwa kwenye maandamano ya amani kupinga uhuni uliofanywa na CCM ya kumpitisha kihuni, kibabe na kuvunja sheria na kanuni kiuwazi kabisa diwani kupitia CCM kuwa Meya wa Jiji la Arusha. Maandamano haya yalilenga kupaza sauti za wengi katika kudai HAKI na kuzitaka mamlaka kuzingatia sheria na kanuni.

CHADEMA Kanda ya Kaskazini, CHADEMA Mkoa wa Arusha pamoja, familia za wote waliofiwa na wapenzi wao na Watanzania wote tunaungana kukumbuka damu za ndugu zetu zilivyomwagika. Ni majonzi makubwa sana na kamwe haitasahaulika katika historia ya mapambano ya kudai utawala wa kidemokrasia katika nchi hii.

CHADEMA tunaendelea na tutaendelea kuenzi tukio hili kwa heshima ya Wakazi wa Jiji la Arusha ambapo wananchi wa Jiji hili walishuhudia uchokozi wa polisi pale walipokuwa katika viwanja vya NMC kwenye mkutano wa hadhara siku hiyo hiyo mabomu yalifyatuliwa na kupelekea maelfu ya wakazi waliokuwa wakifuatilia mkutano huo kutawanyika na kukanyagana uwanjani hapo. Tukio hili lilisababisha majeruhi wengi sana sana. Hata mara baada ya tukio hili wakazi wa Jiji la Arusha ndio waliendelea mara MIA zaidi kuipenda CHADEMA na kuwaamini zaidi viongozi wa chama maana walielewa msingi wa kile tulichokuwa tumekisimamia kama chama, HAKI na UTAWALA WA SHERIA.

Katika maadhimisho haya chama KANDA YA KASKAZINI kinaazimia yafuatayo;
Mwezi wote wa Januari mwaka huu utakuwa mwezi maalumu wa KUHUISHA vuguvugu la kudai katiba mpya katiba ya wananchi na kisha moto wa kudai katiba mpya ya wananchi kuhakikisha unaendelea. Kwa mwenendo wa serikali ya awamu ya tano uhitaji wa katiba mpya ya wananchi umeonekana kwa dhahiri sambamba na kudai tume huru ya uchaguzi.

Chama kitaratibu matukio ya kijamii kwa lengo la kuzifikia familia za wafiwa kama ambavyo imekuwa ikifanya kila mara
Aidha tunatumia siku ya leo kurudia mambo tuliyokwisha kuyasema siku kama ya leo mwaka 2017 ambayo yanakwenda sambamba na maoni na mapendekezo ya TUME YA HAKI ZA BINADABU NA UTAWALA BORA ambao walifanya uchunguzi wa tukio lililopelekea mauaji hayo. Kwa kuangalia mwenendo mzima wa nchi kwa kipindi hiki tunapendekeza na kuishauri serikali kuwa;
Serikali ya awamu ya tano izingatie utawala wa sheria. Kwa bahati mbaya sana kuna mwenendo unaonekana kwa dhahiri kuwa nchi inaendeshwa kimatamko tamko. Nchi kuendeshwa kwa matamko na kauli mbiu maana yake ni kupoteza uelekeo (FOCUS). Tanzania inahitaji kuonekana kuendeshwa kwenye mifumo ya kitaasisi imara na sio mtu mmoja aonekane yeye ndio Imara. Utashi wa mtu mmoja kuendesha mambo ni hatari kwa sababu yatatutoa kwenye kuzingatia katiba na sheria. Haya yanaonekana kwa maneno na matendo kwenye uongozi na utawala wa awamu hii.

Jeshi la polisi lisitumike na lisifanye uadui na vyama vya siasa. Jeshi la polisi hawalali isipokuwa kwa kuwaza CHADEMA au vyama kadhaa vya upinzani watawadhibiti vipi. Picha inayotafsirika kuwa wanatumika na chama tawala kwa maana ya serikali kuua na kugandamiza upinzani. Athari ya muonekano huu ni mbaya maana vyama na wananchi wanaweza kuungana dhidi yao na hivyo kupelekea balaa ambalo majuto yake yatakuwa na gharama kubwa. Hii ni tahadhari.

Serikali ijitathmini mwenendo wake katika kusimamia uchumi. Serikali isijifungie kwenye majedwali ya takwimu wawaangalie wananchi na hali ya kimaisha. Masihara ya kuhusu vyuma kukaza ni mizaha yenye ukweli. Kusema uchumi umekua na kuimarika halafu una benki TANO tena ambazo ni Community Bank zinafilisika haya ni masihara ya kitakwimu.

Serikali ya awamu ya TANO ijifunze kuwa WAVUMILIVU. Uvumilivu ni pamoja na kuwa tayari kusikia wapinzani wako wanasema nini. Kuambiwa kuwa hufanyi vizuri mahali fulani sio DHAMBI na SIO DHAMBI hata kidogo. VIkao vya Bunge vionyeshwe LIVE (MUBASHARA) na wananchi wafuatilie kazi za wabunge wao, aidha maneno ya kukosoa utendaji yasionake kama vile ni uchochezi na kimsingi watarajie kuyasikia mengi maana wananchi hawatanyamaza.

Serikali ya awamu ya tano na kimaalumu sana kwa MHE RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA abatilishe kauli yake ya kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa. Kwa kauli ile hatudhani kama kwa kuzuia mikutano ya hadhara ndio italeta maendeleo kwa haraka, hatudhani. Siasa ni kazi na awaache wanasiasa nao wafanye kazi yao (SPECIALIZATION). Kauli ile ni kinyume kabisa na katiba ya nchi na sheria zetu tulizojiwekea.
Wananchi wa Tanzania wakumbuke na kamwe wasisahau hekima iliyopo kwenye neno hili, Kuuona uovu na kukaa kimya, ukimya huo hugeuka kuwa uovu. Kamwe tusikae kimya na sauti ya mtu mmoja isiposikika iongezeke ya pili na ya tatu mpaka nguvu ya sauti ya wengi isikike, hiyo ndio sauti ya umma yenye nguvu ya umma. Lolote ambalo litafanywa au kuongelewa, kusemwa au kutolewa maagizo na likawa kinyume na katiba, kanuni na sheria na mwenendo wa kiustaarabu wa Utanzania TUSIKAE KIMYA TENA. Jitihada hii iandane sambamba na kuungana pamoja kupiga vita ufisadi na rushwa na wote tuwe walinzi wa rasilimali za nchi.

MWISHO KABISA, USTAARABU NA WELEDI WA UONGOZI KATIKA NCHI NI PALE AMBAPO WADAU WAKUU KATIKA SIASA MNAPATA FURSA YA KUKUTANA NA KUZUNGUMZIA MUSTAKABALI WA MAENDELEO, HALI YA AMANI KATIKA TAIFA NA MWENENDO MZIMA WA MAMBO SERIKALI YA AWAMU YA TANO IONE UMUHIMU HUU HASA KIPINDI HIKI. WELEDI NA USTAARABU HUU UTAONDOA DHANA YA MAJIVUNO YENYE HASARA KWANI WATANIAMBIA NINI HAO. MAZUNGUMZO NI DAWA TOSHA NA MAZUNGUMZO YANAWEZA KUKUPA MENGI USIYOYAJUA.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki CHADEMA na izidi kuimarika zaidi..!

Imetolewa leo
Tarehe 5 Januari 2018
Amani Golugwa
KATIBU CHADEMA KANDA YA KASKAZINI.
Arusha.

0 Comments:

Post a Comment